MAANDAMANO YA CHADEMA YALIYOPANGWA KUFANYIKA LEO YAPIGWA MARUFUKU, MBOWE KUHOJIWA NA POLISI LEO
Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), yaliyotarajiwa kuanza kufanyika leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Jeshi hilo limeonya kuwa maandamano hayo ni batili na ni kinyume cha sheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana makao makuu ya jeshi la Polisi Dar es
Salaam, Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja
alisema jeshi hilo limeanza kupokea taarifa ya chama hicho, kikitaka
kufanya maandamano kuanzia leo. Lakini, alisisitiza kuwa maandamano hayo
hayataruhusiwa.
“Septemba
15 jeshi lilitoa taarifa kuhusu kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe akiwahimiza wafuasi wa chama chake kufanya
maandamano na migomo isiyokoma pote nchini ili kusitishwa kwa Bunge la
Katiba na hivi sasa tumeanza kupokea taarifa ya chama hicho kufanya
maandamano,” alisema.
Alisema
maandamano hayo ni batili, kwa sababu Bunge la Katiba linaloendelea
hivi sasa, linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na
hakuna sheria iliyokiukwa, hivyo kitendo cha kufanya maandamano,
kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume cha sheria, jambo ambalo
jeshi la polisi haliwezi kuruhusu.
Aidha,
alisema kuwa ieleweke wazi kwamba Bunge la Katiba, lipo kisheria na
kila jambo linalofanyika bungeni ni kwa mujibu wa sheria.
Chagonja alisema jeshi la polisi lina jukumu la kulinda watu wote, wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
“Hata
hivyo, hivi sasa kuna kesi inayoendelea Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, inayohoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge hilo na kesi hiyo
haijafikia mwisho na uamuzi kutolewa, hivyo maandamano hayo yaliyopangwa
na Chadema yanaingilia uhuru wa Mahakama, jambo ambalo siyo sahihi.
Mahakama kama chombo cha kutoa haki, kiachwe kifanye kazi yake,” alisema.
Chagonja
alitoa mwito kwa wananchi wote, kuendelea na shughuli zao na yeyote
atakayekiuka katazo hilo, jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua
kali kwa mujibu wa sheria.
Wakati
Chagonja akiyasema hayo, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, amewaonya
wafuasi wa Chadema wanaodaiwa kutaka kuandamana hadi Viwanja vya Bunge
kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, uongozi wa Chadema mkoani humo, umedaiwa kusisitiza maandamano yako palepale.
Akizungumza
jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula alisema
maandamano hayo, pia yamepangwa kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa
Dodoma.
Alisema
juzi walipokea taarifa kutoka kwa Uongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma,
juu ya kufanya maandamano ya amani kuanzia viwanja vya Nyerere Square
hadi viwanja vya Bunge kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana.
Alisema
taarifa ya maandamano kama hayo, yanayotarajia kufanyika katika wilaya
zote za mkoa wa Dodoma, ilitolewa jana ambapo ni muda ulio kinyume na
sheria ya kutoa taarifa za maandamano ndani ya saa 48.
Alisema
katika barua ya chama hicho kwenda kwa Jeshi la Polisi, viongozi wa
Chadema wa Mkoa huo, walisema wanapinga Bunge la Katiba na wanataka
kupaza sauti zao, zisikike dunia nzima na walisisitiza kufanya
maandamano hayo leo.
“Walikuja
hapa viongozi wa Chadema Mkoa, tulikaa nao kwenye mazungumzo zaidi ya
saa mbili, tuliwaambia Bunge lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na hakuna
mahakama iliyotamka Bunge lisitishwe, lakini walisisitiza kuwa
maandamano yako pale pale,” alisema.
“Maandamano
hayo ni batili yanapinga chombo ambacho kipo kwa mujibu wa sheria,
tunasisitiza wananchi wa Dodoma wasishiriki maandamano hayo, hayana tija
hata kidogo na wananchi wasijitokeze waendelee na shughuli zao,” alisema.
Alisema
maandamano ni haki ya kikatiba, lakini wanatakiwa kufuata sheria.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kudhibiti maandamano hayo katika
wilaya zote, kutokana na viongozi wa Chadema kukaidi amri ya kutaka
kusitisha maandamano hayo.
Wakati
jeshi la Polisi likichukua hatua hiyo, Umoja wa Vijana Wazalendo wa
Vyuo vya Elimu ya Juu Dar es Salaam, nao umejitokeza na kulaani kauli
zilizotolewa na Mbowe za kuhamasisha maandamano na migomo nchi nzima,
hata kama jeshi la Polisi halitabariki kufanyika kwa mambo hayo.
Mwenyekiti
wa Umoja huo, Mussa Omar anayesoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),
alisema umoja huo ni Muungano wa vyuo 14 vya elimu ya juu vilivyopo
Dar es Salaam.
Alisema
Watanzania wengi wamekerwa na kusononeshwa na kauli ya kiongozi huyo ya
kuhamasisha maandamano, alizozitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu
wa uchaguzi wa Chadema, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Tumemsikia
akiahidi maandamano bila kikomo kwa kibali cha polisi au bila kibali
cha polisi mbele ya wajumbe na wageni ambao wengine sio Watanzania,” alisema Omar.
Aliongeza kuwa kauli kama hiyo, haiwezi kusemwa hata na Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Alimtaka
Mbowe afahamu dhamana kubwa ya uongozi aliyonayo kwa wafuasi wake na
Watanzania kwa ujumla, wakimtaka afuate misingi ya sheria za nchi,
katiba na utawala bora.
Pia,
alisema kauli zilizotolewa na Mbowe, hazibebeki na mtu yeyote katika
taifa hili, kwani alitoa kauli mbaya kuliko zote kisiasa, ambazo
zimewahi kusemwa majukwaani.
“Watanzania
tukikaa bila kuzilaani na kuzikemea kauli zake tutakuwa hatujitendei
haki sisi wenyewe na pia hatuvitendei haki vizazi vijzvyo vya nchi
yetu,” aliongeza.
Alihoji uhalali wa kutoa amri hizo kwa wafuasi wake, ilhali ni kiongozi tu wa chama, tena ambacho hakiko madarakani.
Alisema
Watanzania wanapaswa kuwakataa viongozi wenye jazba na kutumia mabavu
katika kutimiza majukumu yao, kwani wanaweza kuiingiza nchi katika
vurugu zisizo na ulazima.
Pia
alivitaka vyombo vya dola, visizivumilie kauli kama hizo, zilizotolewa
na Mbowe, kwani vyombo vya dola vina dhamana ya kulinda, kutunza na
kuendeleza amani na utulivu wa nchini, wachukue hatua kali za kisheria
kwa kauli ya kutishia uvunjifu wa amani kabla hajaingiza nchi kwenye
machafuko ya kisiasa.
Wakati
huo huo, viongozi wa juu wa chama hicho, leo wamepanga kumsindikiza
Mbowe kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, ambako ameitwa kwa
barua.
Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema Mbowe alipokea barua,
ikimtaka afike Makako Makuu ya jeshi hilo leo saa 5:00 asubuhi.
“Mwenyekiti
wetu ameitwa Makao Makuu ya Polisi leo na hatujui kaitiwa nini, huenda
anakwenda kuhojiwa na huenda mwito huo umetokana na kauli alizotoa
awali katika mkutano mkuu, ambazo zililenga kuhamasisha maandamano ya
nchi nzima kupinga Bunge la Katiba linaloendelea”, alisema Dk Slaa.
Alitaja
watakaoongoza msafara wa amani wa kumsindikiza Mbowe kuwa ni
mwanasheria wao, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Makamu
Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Safari na Mwanasheria
Peter
Kibatala.
Hata
hivyo, alisema pamoja na kiongozi huyo kuitwa na polisi, bado jeshi
hilo haliwezi kuvunja ajenda ya kuandamana, kwa kuwa ilipitishwa na
Kamati Kuu ya chama hicho, na kwamba polisi wao wanapaswa kutoa kibali
cha kuruhusu maandamano hayo.
Awali,
alisema maazimio yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho ni
kuunganisha nguvu ya pamoja na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) .
Alisema maazimio hayo, yataanza Desemba 14, mwaka huu, siku ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa unaanza.
Alieleza
kwamba chama hicho kimeunda kamati ya watu watano, itakayoangalia jinsi
ushirikiano wa Ukawa utakavyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutoka kwao nje bungeni, kulikuwa sahihi. Alisema katiba mpya, haiwezi kupatikana leo au kesho.
No comments:
Post a Comment