Hii kali ya mwaka!!
Mwanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe atangaza nia kuwania urais CCM
Hamasa ya wanaCCM kutangaza nia ya kuwania urais imemwibua mwanafunzi Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Maliki Malupu (34). Malupu alitangaza nia ya...
kugombea urais kupitia CCM akiahidi kushughulikia suala la elimu, afya, kilimo na michezo huku akijua kuwa umri wake haujatimia miaka 40 inayotakiwa kikatiba.
Akitangaza nia hiyo mjini Morogoro jana, Malupu
alisema kutokana na uaminifu na uadilifu wake, ameamua kuwania nafasi
hiyo pamoja na mambo mengine kwa kuwa ni haki yake kikatiba.
Alipoulizwa atatimizaje nia yake hiyo bila kuwa na
sifa kikatiba, alisema vifungu vya katiba vinavyotaja umri vina utata,
hivyo ameamua kuingia kuvitafutia suluhisho.
“Unajua ibara ya 39 (1) (b) inasema lazima utimize
miaka 40, lakini ibara (d) inasema mtu mwenye sifa za kuwa mbunge au
mjumbe wa baraza la wawakilishi anaweza kuwania urais,” alisema
akifafanua kuwa yeye ana sifa hizo.
Akieleza sababu nyingine zilizomsukuma kuwania
urais, Malupu alisema kuwa ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa
kikamilifu kwa kuwa muda mrefu imekuwa ikichezewa na baadhi ya viongozi.
Alisema muundo wa sekta hiyo unapaswa kurekebishwa kwa ama kufutwa au kuondoshwa utaratibu wa kupanga
viwango vya ufaulu wa GPA kwa wanafunzi wa elimu ya sekondari katika
mitihani ya kidato cha sita na cha nne.
Alisema utaratibu huo haufai kwa kuwa hautoi
matokeo ya kuboresha maarifa kwa wanafunzi, pia unawaathiri wanafunzi
kisaikolojia katika kujitofautisha wao na wanafunzi wa elimu ya juu.
“Nitahakikisha naboresha mitalaa kwa masomo ya
kidato cha nne na cha sita ili kuleta weledi wa kina na wa kutosha,
nitaboresha mazingira ya watumishi sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na
kuboresha mishahara na stahiki za walimu wa msingi hadi vyuo,” alisema.
Katika mkutano wake wa saa 1.30, Malupu alisema
atahakikisha anadhibiti suala la maprofesa kuacha kazi yao ya weledi na
kukimbilia katika siasa na ataboresha stahiki zao na mishahara kwa
kuwalipa vizuri wanaofundisha vyuo vya Serikali na binafsi bila ubaguzi
wowote ili kuimarisha sekta ya elimu ngazi vyuo vikuu.
Malupu alisema ataitazama sekta ya kilimo kwa
kuongeza vyuo vikuu vya kilimo ili kuleta tija ya kilimo katika sekta
hiyo na Serikali yake itakuwa na mkakati mahsusi wa kutoa elimu na
mitaji kwa wakulima wanaofanya kilimo chenye tija na kilimo cha
kujikimu. Katika afya, Malupu alisema kuwa atahakikisha suala la afya
linasimamiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja kuwapatia wazee huduma bure na
kwamba zahanati, vituo vya afya na hospitali zinapatiwa vifaatiba vya
kutosha ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.
Malupu pia alizungumzia wananchi wanaoishi katika
visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza na Mafia mkoani Pwani kuwa
wamesahaulika, hivyo akiteuliwa na baadaye kuchaguliwa atahakikisha
anakifanya kisiwa cha Ukerewe kuwa mkoa unaojitegemea ili kuwapunguzia
wananchi umbali wa kufuata huduma Mwanza.
No comments:
Post a Comment